John 1

 

 

 

1 Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.
2 Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
3 Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
4 Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
5 Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
6 Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane,
7 ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini.
8 Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
9 Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
10 Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua.
11 Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.
12 Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.
13 Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao.
14 Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
15 Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: <Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.">


16 Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
17 Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo.
18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
19 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?"
20 Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, "Mimi siye Kristo."
21 Hapo wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?" Yohane akajibu, "La, mimi siye." Wakamwuliza, "Je, wewe ni yule nabii?" Yohane akawajibu, "La!"
22 Nao wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma."
23 Yohane akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: <Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana.">
24 Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.
25 Basi, wakamwuliza Yohane, "Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?"
26 Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
27 Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake."
28 Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.


29 Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
30 Huyu ndiye niliyesema juu yake: <Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!>
31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua."
32 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.

33 Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: <Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.>
34 Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu."
35 Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
36 Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu."
37 Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
38 Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?"
39 Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.
40 Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
41 Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha" (maana yake Kristo).
42 Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani, "Mwamba.")


43 Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, "Nifuate."
44 Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.
45 Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, "Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti."
46 Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?" Filipo akamwambia, "Njoo uone."
47 Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, "Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake."
48 Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje kunijua?" Yesu akamwambia, "Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona."
49 Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!"
50 Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya."
51 Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu."


John 2

 

 

1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo,
2 naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
3 Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!"
4 Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado."
5 Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni."
6 Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha.


7 Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji." Nao wakaijaza mpaka juu.
8 Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu."
9 Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi,
10 akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!"
11 Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
12 Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache.

13 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda Yerusalemu.
14 Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng'ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.


15 Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo na ng'ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao.
16 Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!"
17 Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu kwa nyumba yako waniua."
18 Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?"
19 Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu."
20 Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?"
21 Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake.
22 Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema Yesu.
23 Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizozifanya.
24 Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote.
25 Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.

 

John 3

 

 

 

1 Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo, jina lake Nikodemo.
2 Siku moja alimwendea Yesu usiku, akamwambia, "Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye."
3 Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza kuuona ufalme wa Mungu."
4 Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili!"
5 Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.
6 Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho.
7 Usistaajabu kwamba nimekwambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya.
8 Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho."
9 Nikodemo akamwuliza, "Mambo haya yanawezekanaje?"
10 Yesu akamjibu, "Je, wewe ni mwalimu katika Israel na huyajui mambo haya?
11 Kweli nakwambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini ninyi hamkubali ujumbe wetu.
12 Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini nikiwaambieni mambo ya mbinguni?
13 Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu ambaye ameshuka kutoka mbinguni.
14 "Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo,


15 ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele.
16 Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
17 Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe ulimwengu.
18 "Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu.
19 Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu.
20 Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe.
21 Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu."
22 Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake. Alikaa huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu.
23 Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza.
24 (Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.)
25 Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja kuhusu desturi za kutawadha.
26 Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, "Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea."
27 Yohane akawaambia, "Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu.
28 Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: <Mimi siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!>
29 Bibiarusi ni wake bwanaarusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa.
30 Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue.
31 "Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wote.
32 Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali ujumbe wake.
33 Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu ni kweli.
34 Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia mtu huyo Roho wake bila kipimo.
35 Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote.
36 Anayemwamini Mwana anao uzima wa milele; asiyemtii Mwana hatakuwa na uzima wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake."

 

John 4

 

 

1 Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane.
2 (Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.)
3 Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya;
4 na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria.
5 Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu.
6 Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
7 Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, "Nipatie maji ninywe."
8 (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)
9 Lakini huyo mwanamke akamwambia, "Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?" (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu.)
10 Yesu akamjibu, "Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia: <Nipatie maji ninywe,> ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo hai."
11 Huyo mama akasema, "Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai?
12 Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa maji ya kisima hiki."
13 Yesu akamjibu, "Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena.
14 Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima wa milele."
15 Huyo mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji."
16 Yesu akamwambia, "Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa."
17 Huyo mwanamke akamwambia, "Mimi sina mume." Yesu akamwambia, "Umesema kweli, kwamba huna mume.
18 Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli."
19 Huyo Mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii.


20 Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu."
21 Yesu akamwambia, "Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu.
22 Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi.
23 Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli, watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba anaotaka.
24 Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho wake."
25 Huyo mama akamwambia, "Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu."
26 Yesu akamwambia, "Mimi ninayesema nawe, ndiye."
27 Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: "Unataka nini?" au, "Kwa nini unaongea na mwanamke?"
28 Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,
29 "Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?"
30 Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.
31 Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: "Mwalimu, ule chakula."
32 Lakini Yesu akawaambia, "Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi."
33 Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula?"
34 Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.
35 Ninyi mwasema: <Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!> Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa.
36 Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.
37 Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: <Mmoja hupanda na mwingine huvuna.>
38 Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao."
39 Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: "Ameniambia mambo yote niliyofanya."
40 Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili.
41 Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake.
42 Wakamwambia yule mama, "Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu."
43 Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya.
44 Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, "Nabii hapati heshima katika nchi yake."
45 Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo.
46 Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu.
47 Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi.
48 Yesu akamwambia, "Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!"
49 Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa."
50 Yesu akamwambia, "Nenda tu, mwanao yu mzima." Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake.
51 Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima.
52 Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, "Jana saa saba mchana, homa ilimwacha."
53 Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: "Mwanao yu mzima." Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote.
54 Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.

 

John 5

 

 

1 Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu.
2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao.
3 Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza. Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe,
4 maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.
5 Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane.
6 Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo, akatambua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, "Je, wataka kupona?"
7 Naye akajibu, "Mheshimiwa, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia."


8 Yesu akamwambia, "Inuka, chukua mkeka wako utembee."
9 Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.
10 Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, "Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako."
11 Lakini yeye akawaambia, "Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: <Chukua mkeka wako, tembea.">
12 Nao wakamwuliza, "Huyo mtu aliyekwambia: <Chukua mkeka wako, tembea,> ni nani?"
13 Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu.
14 Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa Hekaluni, akamwambia, "Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi."
15 Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya.
16 Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu.
17 Basi, Yesu akawaambia, "Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi."
18 Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumwua Yesu: si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.
19 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile.
20 Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu.
21 Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uzima wale anaopenda.
22 Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana,
23 ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.
24 "Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uzima wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo na kuingia katika uzima.
25 Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi.
26 Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanawe kuwa asili ya uhai.
27 Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu.
28 Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake,
29 nao watafufuka: wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa.
30 "Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi nina hukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.
31 Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli.
32 Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli.
33 Ninyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli.
34 Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa.
35 Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo.
36 Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma.
37 Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Ninyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake,
38 na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma.


39 Ninyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uzima wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia!
40 Hata hivyo, ninyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uzima.
41 "Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu.
42 Lakini nawajua ninyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu.
43 Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea.
44 Mwawezaje kuamini, hali ninyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu ninyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu?
45 Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye ninyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki.
46 Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia; maana Mose aliandika juu yangu.
47 Lakini hamuyaamini yale aliyoandika, mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?"

 

John 6

 

 

1 Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au Ziwa Tiberia).
2 Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa.
3 Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake.
4 Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia.
5 Basi, Yesu na alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, "Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?"
6 (Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.)
7 Filipo akamjibu, "Mikate ya denari mia mbili za fedha haiwatoshi watu hawa hata kama ila mmoja atapata kipande kidogo tu!"


8 Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia,
9 "Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?"
10 Yesu akasema, "Waketisheni watu." Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume elfu tano.
11 Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka.
12 Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee."
13 Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili.
14 Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, "Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni."
15 Yesu akajua ya kuwa watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake.
16 Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani,
17 wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado.


18 Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.
19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana.
20 Yesu akawaambia, "Ni mimi, msiogope!"
21 Walifurahi kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walipokuwa wanakwenda.
22 Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao.
23 Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu.
24 Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta.
25 Wale watu walipomkuta Yesu ng'ambo ya pili wa ziwa walimwuliza, "Mwalimu, ulifika lini hapa?"
26 Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
27 Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishugulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uzima wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho."
28 Wao wakamwuliza, "Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?"
29 Yesu akawajibu, "Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu muifanye: kumwamini yule aliyemtuma."

30 Hapo wakamwambia, "Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani?
31 Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: <Aliwalisha mkate kutoka mbinguni.">
32 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye ninyi mkate halisi kutoka mbinguni.
33 Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uzima."
34 Basi, wakamwambia, "Mheshimiwa, tupe daima mkate huo."
35 Yesu akawaambia, "Mimi ndimi mkate wa uzima. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
36 Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini.
37 Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu,
38 kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.
39 Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote Siku ya mwisho.
40 Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele; nami nitamfufua Siku ya mwisho."
41 Basi, Wayahudi wakaanza kunung'unika kwa kuwa alisema: "Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni."
42 Wakasema, "Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunawajua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?"
43 Yesu akawaambia, "Acheni kunung'unika ninyi kwa ninyi.
44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo Siku ya mwisho.
45 Manabii wameandika: <Watu wote watafundishwa na Mungu.> Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu.
46 Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.
47 Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uzima wa milele.
48 Mimi ni mkate wa uzima.
49 Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa.
50 Huu ndio mkate kutoka mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa.
51 Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu."
52 Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao:
53 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uzima ndani yenu.
54 Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake.
57 Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu.
58 Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zetu, wakafa. Aulaye mkate huu ataishi milele."
59 Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu.
60 Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, "Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?"
61 Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananung'unika juu ya jambo hilo, akawauliza, "Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka?
62 Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza?
63 Roho ndiye atiaye uzima; binadamu peke yake hawezi. Maneno niliyowaambieni ni Roho, ni uzima.
64 Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini." (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti.)
65 Kisha akasema, "Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu."
66 Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma wasiandamane naye tena.
67 Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, "Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?"
68 Simoni Petro akamjibu, "Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno yaletayo uzima wa milele.
69 Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu."
70 Yesu akawaambia, "Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!"
71 Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili.


John 7

 

 

1 Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya. Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumwua.
2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
3 Basi ndugu zake wakamwambia, "Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya.
4 Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadam unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu."
5 (Hata ndugu zake hawakumwamini!)
6 Basi, Yesu akawaambia, "Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa.
7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nauambia wazi kwamba matendo yake ni maovu.
8 Ninyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika."
9 Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya.
10 Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri.
11 Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; Wakauliza: "Yuko wapi?"
12 Kulikuwa na minong'ono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, "Ni mtu mwema." Wengine walisema, "La! Anawapotosha watu."
13 Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
14 Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda Hekaluni, akaanza kufundisha.
15 Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema "Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?"
16 Hapo Yesu akawajibu, "Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.
17 Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.
18 Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote.
19 Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?"
20 Hapo watu wakamjibu, "Una wazimu wewe! Nani anataka kukuua?"
21 Yesu akawajibu, "Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia.
22 Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa ninyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato.
23 Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi Sheria ya Mose isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato?
24 Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki."
25 Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, "Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu?
26 Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo?
27 Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!"
28 Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema, "Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui.
29 Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma."
30 Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.


31 Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, "Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?"
32 Mafarisayo waliwasikia watu wakinong'ona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni.
33 Yesu akasema, "Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma.
34 Mtanitafuta lakini hamtaniona, maana pale nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika."
35 Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, "Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki?
36 Ana maana gani anaposema: <Mtanitafuta lakini hamtanipata, na mahali nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika?">
37 Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalum. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, "Aliye na kiu na aje kwangu anywe.
38 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: <Anayeniamini mimi, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka moyoni mwake!">
39 (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.)
40 Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, "Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!"
41 Wengine wakasema, "Huyu ndiye Kristo!" Lakini wengine walisema, "Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya?
42 Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: <Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!">
43 Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu.
44 Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.
45 Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, "Kwa nini hamkumleta?"
46 Walinzi wakawajibu, "Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!"
47 Mafarisayo wakawauliza, "Je, nanyi pia mmedanganyika?
48 Je, mmekwisha mwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini?
49 Lakini umati huu haujui Sheria ya Mose; umelaaniwa!"
50 Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia,
51 "Je, Sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?"
52 Nao wakamjibu, "Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!"
53 Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda zake;


go to chapters........1-7.......8-14.......15-18.......19-21

BOOK OF JOHN HOMEPAGE